Mahakama moja ya Russia, imeamuru kukamatwa kwa Yulia Navalnaya bila kuwepo mahakamani kwa madai ya kushiriki katika shughuli za kundi la itikadi kali.
Navalnaya ni mjane wa Alexey Navalny, ambaye alikuwa mpinzani mkuu wa Rais wa Russia, Vladimir Putin.
Navalny alifariki katika gereza la Arctic mwezi Februari alipokuwa akitumikia kifungo cha miaka 19 kwa makosa ya itikadi kali.
Navalnaya ameahidi kuendelea na kazi ya marehemu mumewe. Amri ya mahakama ina maana kwamba Navalnaya, ambaye anaishi uhamishoni angekamatwa endapo angeingia Russia.
“Unapoandika kuhusu hili, tafadhali usisahau kuandika jambo kuu, Vladimir Putin ni muuaji na mhalifu wa kivita,” aliandika Navalnaya kwenye mtandao wa X.
“Mahali pake ni gerezani, na sio mahali pengine huko The Hague,” aliandika mjane huyo na kumshutumu rais wa Russia, kwa mauaji ya mumewe.
Lakini Russia, imekana kuhusika na kifo cha Navalny.