Mkataba wa kusitisha mapigano Sudan Kusini umevunjika

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir, (C) na kiongozi wa upinzani Riek Machar wakipeana mikono ya kutakiana amani, Juni 21,2018

Mkataba wa kusitisha mapigano uliotiwa saini na Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na waasi ulikiukwa Jumamosi ikiwa ni saa chache baada ya utekelezwaji wake huku pande zote zikishutumiana kwa kufanya mashambulizi katika taifa hilo changa duniani.

Msemaji wa waasi Lam Paul Gabriel alivishutumu vikosi vya serikali kwa kushambulia maeneo ya waasi yaliopo nje ya kusini-magharibi mwa mji wa Wau huko Sudan Kusini, takribani saa sita baada ya usitishwaji mapigano kuanza.

Wakati huo huo msemaji wa serikali Ateny Wek Ateny aliliambia shirika la habari la Associated Press-AP kwamba upinzani ulishambuliwa “wana uongozi huru. Hawadhibitiwi na mtu yeyote”.

Riek Machar (L) na Rais Salva Kiir wakiwa mjini Juba, Sudan Kusini

Rais Kiir na mpinzani wake Riek Machar ambaye alikuwa msaidizi wa zamani wa Kiir walitia saini mkataba wa kusitisha mapigano siku ya Jumatano baada ya mazungumzo ya ana kwa ana yaliyofanyika katika nchi jirani kwenye mji mkuu wa Sudan, Khartoum. Mkataba huo unatoa wito wa kufunguliwa njia za barabara kwa ajili ya kufikisha msaada wa kibinadamu, kuachiwa huru kwa wafungwa na kuondoa vikosi vya jeshi kulingana na shirika la habari la SUNA. Shirika hilo la SUNA pia liliripoti vikosi vya jeshi na Umoja wa Afrika na kundi la IGAD watafuatilia usitishaji huo wa mapigano.

Maelfu ya watu wameuwawa tangu vilipoanza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan Kusini mwaka 2013 chini ya miaka miwili baada ya nchi hiyo kujipatia uhuru wake kutoka Sudan. Mzozo huo pia umewalazimisha watu milioni tatu kukimbia nyumba zao.