Hata hivyo, wizara ya afya ya Gaza chini ya utawala wa Hamas imeripoti Jumamosi kwamba zaidi ya watu 27,000 waliuawa na zaidi ya 66,000 walijeruhiwa huko Gaza tangu shambulio la Hamas la Oktoba 7 dhidi ya Israel.
Umoja wa Falme za Kiarabu umetenga dola milioni 5 kama msaada kwa shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi wa Palestina ( UNRWA). Baadhi ya nchi zilisitisha michango yao kwa shirika hilo baada ya taarifa kuibuka kuwa wafanyakazi wake 12 walishiriki katika shambulio la Oktoba 7.
Mapigano yaliendelea Ijumaa huko Gaza, huku maafisa wa afya katika eneo hilo wakisema kwamba watu 105 waliuawa usiku kucha, kulingana na shirika la habari la AFP.
AFP imeinukuu idara ya habari ya Hamas ikisema mashambulizi ya anga na mizinga ya Israel yaliulenga mji wa kusini mwa Gaza wa Khan Younis.
Reuters iliripoti Ijumaa kwamba jeshi la Israel lilishambulia kwa makombora vitongoji vya Rafah kusini mwa Gaza, ambako maelfu ya Wapalestina walikimbilia tangu Israel ilipoanza kuushambulia mji wa Khan Younis.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva Ijumaa, msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, Jens Laerke, alielezea wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa mapigano huko Khan Younis na kuongezeka kwa idadi ya watu wanaokimbilia Rafah.