Upande wa mashariki na kaskazini magharibi mwa mji mkuu, ndege za kivita zililenga ngome za kikosi cha dharura cha RSF ambacho kilijibu kwa kutumia silaha za kupambana na ndege, mashahidi wameliambia shirika la habari la AFP.
Kundi la kitongoji cha eneo hilo limesema watu watano waliuawa na wengine 17 kujeruhiwa katika mlipuko uliotokea Ombada, kaskazini magharibi mwa Khartoum, lakini idadi ya waliofariki huenda ikaongezeka kwa sababu majeruhi zaidi walitolewa kutoka kwenye vifusi.
Ndege zisizo na rubani za kikosi cha RSF zililenga hospitali kubwa ya kijeshi, kulingana na mashahidi. Shambulio kama hilo siku ya Jumamosi kwenye hospitali hiyo liliua watu watano na kujeruhi wengine 22, jeshi lilisema.
Vita kati ya mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na makamu wake wa zamani, kamanda wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo, vimeua watu 3,000, kulingana na shirika lisilo la kiserikali linalofuatilia migogoro (ACLED), lakini idadi ya waliouawa katika vita hivyo inaaminika kuwa kubwa zaidi.
Watu wengine milioni 3 ni wakimbizi wa ndani au walivuka mipaka na kukimbilia katika nchi jirani, kulingana na shirika la kimataifa la uhamiaji.