Misri imetuma ujumbe wa ngazi ya juu Israel, Ijumaa kwa matumaini ya kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano na Hamas, Gaza, maafisa wawili wamesema.
Wakati huo huo, imeonya uwezekano wa mashambulizi ya Israel kuulenga mji wa Rafah, kwenye mpaka na Misri, na inaweza kuleta athari mbaya kwa utulivu wa kikanda.
Afisa mkuu wa ujasusi wa Misri, Abbas Kamel, anaongoza ujumbe na anapanga kujadili na Israel mpango mpya wa kusitisha mapigano kwa muda mrefu Gaza, afisa wa Misri amesema, kwa sharti la kutotajwa ili kueleza hayo kwa uhuru.
Wakati vita vikiendelea na majeruhi kuongezeka, kumekuwa na shinikizo la kimataifa kwa Hamas na Israel kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano. Mazungumzo ya Ijumaa yatalenga kwanza juu ya ubadilishanaji mdogo wa mateka wanaoshikiliwa na Hamas kwa wafungwa wa Kipalestina, na kurejea kwa idadi kubwa ya Wapalestina.