Mahakama ya Misri Jumanne ilimuhukumu Patrick Zaki, mtafiti wa haki za binadamu ambaye alikuwa akisoma nchini Italy, kifungo cha miaka mitatu jela kwa kusambaza habari za uongo, shirika la kutetea haki Egypt Initiative for Personal Rights(EIPR) na chanzo cha mahakama wamesema.
Zaki alikamatwa wakati wa ziara nchini Misri mwezi Februari 2020, alipokuwa mwanafunzi aliyehitimu katika chuo kikuu cha Bologna. Alishtakiwa kwa kusambaza habari za uongo katika makala aliyoandika kuhusu hali ngumu ya Wakristo wa Misri.
Alikaa jela miezi 22 kabla ya kuachiliwa, akisubiri kukamilika kwa kesi yake katika mahakama ya dharura ya serikali kuhusu masuala ya usalama, katika mji alikozaliwa wa Mansoura.
Hukumu hiyo haina rufaa katika mahakama kuu, lakini inaweza kuidhinishwa au kubatilishwa na rais.
Zaki alifanya kazi kama mtafiti kwenye shirika la EIPR, kundi huru linaloongoza kwa kutetea haki za binadamu, ambalo linasema aliteswa baada ya kukamatwa kwake.