Misri yapunguza nakisi katika bajeti yake

Waziri wa Fedha wa Misri, Samir Radwan.

Serikali ya Misri haitaomba msaada wa fedha kutoka Benki ya Dunia na IMF

Misri inasema imepunguza nakisi katika bajeti yake kwa mwaka ujao wa fedha na hivi sasa haitaomba msaada wa kimataifa wa fedha kusaidia kulipia operesheni za serikali.

Uchumi wa Misri ulipata pigo kubwa wakati wa ghasia za kisiasa ambazo ziliuangusha utawala wa Rais Hosni Mubarak mwezi Februari, huku watalii wa kigeni wakibakia makwao na wafanyakazi wengi wa Misri walivuruga shughuli za biashara kwa maandamano yao kuhusu malipo na hali nzuri makazini.

Maafisa wa Misri waliomba kiasi cha dola bilioni 6.2 kutoka Benki ya Dunia na Shirika la Kimataifa la Fedha Duniani - IMF - ili kusaidia kufadhili operesheni za serikala kwa mwaka wa fedha unaoanza Julai mosi. Lakini Waziri wa Fedha, Samir Radwan amesema Jumamosi kwamba serikalli yake imefanya tathmini ya bajeti na kupunguza nakisi kwa kiwango ambacho hawatahitaji msaada wa fedha kutoka Benki ya Dunia na IMF.

Bwana Radwan amekaririwa na shirika la habari la Reuters akisema kuwa serikali imepunguza nakisi yake kutoka dola bilioni 86 hadi dola bilioni 82. bajeti ya awali ilitabiriwa kuwa na nakisi ya zaidi ya dola bilioni 28, idadi ambayo hivi sasa imepunguzwa kwa dola bilioni sita.

Radwan amesema matokeo yake ni kwamba Misri haihitaji tena msaada wa Benki ya Dunia na IMF, lakini itakubali misaada kutoka mataifa mengine ya kiarabu. Amesema Qatar imeipa Misri dola milioni 500 ambazo amezielezea ni zawadi.