Miili iliyofukuliwa Kenya inafanyiwa vipimo vya vinasaba

Paul Makenci, anayedaiwa kuelekeza waumini kujinyima chakula na maji hadi wafe ili wakutane na mwenyezi mungu, alipofikishwa mahakamani April 17, 2023

Maafisa nchini Kenya wameanza kufanya uchunguzi wa miili ya zaidi ya watu 100 iliyofukuliwa baada ya kuzikwa katika mazingira ya kutatanisha huko Kilifi, pwani ya nchi hiyo.

Watu hao wanaripotiwa kufariki baada ya kujinyima chakula na maji kwa imani ya kidini kuwa watakwenda mbinguni.

Maafisa wamepata miili kadhaa iliyozikwa katika msitu wa Shakahola.

Baadhi ya watu waliokolewa wakiwa hai, na wengine walifariki wakiwa njiani kupelekwa hospitali.

Idadi kubwa ya waliofariki ni watoto.

Watu hao walikuwa wakipata mafunzo kutoka kwa Paul Mackenzie Nthenge, ambaye kabla ya kuanza mahubiri yake yenye utata, alikuwa mwendesha magari. Anazuiliwa na polisi, na inaripotiwa kwamba amekataa kula wala kunywa.

Uchunguzi wa vinasaba yani DNA, utafanyiwa maiti hao na kulinganisha na watu kutoka familia ambazo zimedai kutoweka kwa watu wao. Zaidi ya watu 300 wanaripotiwa kutojulikana walipo na huenda ni miongoni mwa miili inayofukuliwa.