Midahalo ya wagombea urais wa Marekani kuboreshwa

Rais wa Marekani, Donald Trump (kushoto) na mgombea wa chama cha Democratic, Joe Biden, (kulia) wakiwa katika mdahalo wa kwanza wa wagombea urais wa Marekani, Septemba 29.

Taasisi huru inayosimamia mdahalo wa wagombea urais wa Marekani, Jumatano imesema itarekebisha utaratatibu wa mdahalo.

Hatua hiyo ni baada ya malalamiko kutolewa kuhusu mdahalo wa kwanza wa Jumanne kati ya rais Donald Trump, na mpinzani wake Joe Biden.

Mdahalo huo umetajwa na wengi kuwa mdahalo mbaya zaidi katika historia ya siasa za marekani.

Wagombea wawili mara kwa mara waliingiliana au kuzungumza kwa wakati mmoja, na muongoza mudahalo Chris Wallace, mwanahabari wa televijeni ya Fox News, alikemea kwa kutozingatiwa kanuni.

Kamati ya midahalo ya wagombea urais imesema mapungufu yalioonekana katika mdahalo wa kwanza yameonyesha umuhimu wa kuwa na muundo wa ziada ili kuruhusu majadiliano.

Kamati hiyo imempongeza mwanahabari Chris Wallace, namna alivyoongoza mdahalo uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Cleveland, Ohio.

Lakini kamati hiyo imesema itaweka utaratibu mpya kabla ya mdahalo wa pili na watatu ambayo imepangwa kufanyika Oktoba 15 na 22.