Mkuu wa kamisheni ya haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet amelaani ukatili unaofanyika katika jimbo la kaskazini la Ethiopia la Tigray kufuatia ripoti mpya ya pamoja kati ya Umoja wa Mataifa na Ethiopia inayoonya juu ya uwezekano kwamba uhalifu dhidi ya binadamu umefanywa na pande zote.
Akizungumza mjini Geneva leo Jumatano Michelle Bachelet amezihimiza pande zote kuitikia wito wa kimataifa wa kukomesha ukatili na unyanyasaji wote katika jimbo hilo.
Ripoti hiyo ya ushirikiano nadra kati ya ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa na tume ya haki za kibinadamu ya Ethiopia iliyoundwa na serikali ilitolewa siku moja kabla ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu kuanza vita hivyo katika nchi ya pili barani Afrika yenye watu wengi zaidi.
Umoja wa Mataifa uliliambia shirika la habari la Associated Press kwamba ushirikiano huo ulikuwa muhimu kwa timu yake kufikia eneo lenye matatizo ambapo maafisa wa usalama wa Ethiopia kwa kiasi kikubwa wamewazuia waandishi wa habari, makundi ya haki, na waangalizi wengine wa nje kuingia.