Miaka mitatu ya serikali ya mseto Kenya

  • Mwai Gikonyo

Wakenya wakibeba mabango kutaka haki itendeke tangu ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007. Changa moto kuu inayoikabili serikali ya mseto

Februari 28 ni siku ya kuadhimisha miaka mitatu tangu kuundwa kwa serikali ya mseto nchini Kenya, iliyotokana na upatanishi baada ya ghasia kufuatia uchaguzi mkuu wa 2007.

Ni zaidi kidogo ya miaka mitatu tangu matokeo ya uchaguzi yaliyokua na utata mkubwa kati ya rais Mwai Kibaki na waziri mkuu Raila Odinga yaliyosababisha mapigano makali kabisa ya kikabila kushuhudiwa Kenya tangu uhuru wake.

Miaka mitatu baadae, mahasimu hao wawili wametumia muda mkubwa kujaribu kupitisha mageuzi ya kisiasa na kiuchumi ili kuepusha kurudia tena ghasia zilizotokea mwaka 2008.

Wachambuzi wa mambo pamoja na wanaharakati, wanasema ingawa kuna hatua muhimu zimefikiwa lakini, kuna changa moto nyingi zilizobaki. Wakati huo huo, wanasiasa wameanza kujitayarisha kwa uchaguzi mkuu hapo mwaka 2012.

Rais Kibaki anatazamiwa kukamilisha mhula wake hapo mwakani, na waziri mkuu Odinga anatarajiwa na wengi kuwa rais mpya wa Kenya. Lakini waziri huyo mkuu, katika miezi ya hivi karibuni, amekuwa akishambuliwa na pande zote wakati mahasimu wa muda mrefu na washirika wa zamani wanajitayarisha kwa uchaguzi huo.