Mhubiri mashuhuri Graham afariki Marekani

Mhubiri wa Marekani Billy Grahama (Kushoto) akihubiri katika viwanja vya Helsingfors huko Finland Juni 1954.

Billy Graham, mhubiri mashuhuri wa dini ya Kikristo nchini Marekani ambaye mahubiri yake yalikuwa yanawafikia mamilioni ya watu duniani amefariki akiwa na umri wa miaka 99.

Kiongozi huyo alifanya maombi na kuwapa nasaha watu mashuhuri na wenye nguvu wa karne ya 21, tangu wakati wa utawala wa Rais Harry Truman mpaka Barack Obama.

Graham alikuwa kiongozi mwenye kuwavutia wengi, wataalamu wa dini wanasema, wakitaja kuwa ni kati ya wahubiri wachache wenye uwezo wa kuepuka udini na kuweza kuwafikia Wamarekani wengi.

Mnamo mwaka 1950, aliunda Umoja wa Wahubiri wa Billy Graham katika juhudi za kusambaza neno la Mungu kupitia kile kilichokuja kuwa maarufu hivi leo kama “crusades”, mahubiri ya mfululizo ambayo hufanyika katika viwanja mbalimbali.

Graham aliendesha mahubiri haya katika mabara yote isipokuwa Antarctica, akihubiri yeye mwenyewe kupitia matangazo ya satellite. Alihubiri katika mataifa ya Soviet kabla ya kuanguka kwa ukomunisti.

Na katika msimu wa baridi mwaka 1994, Billy Graham alitoa mahubiri huko China na Korea Kaskazini, ambako alikutana na viongozi wa kisiasa na kidini katika nchi hizo.

Kutokana na safari zake alizofanya katika mataifa mbali mbali ulimwenguni, mhubiri huyu mashuhuri wa Marekani alitoa fatwa kuwa Ukristo sio tu dini ya nchi za Magharibi.

“Ni wenye nguvu Afrika na Amerika ya kati na Asia kuliko ilivyo nchi za Ulaya, kwa hatua kubwa. Huko Ulaya , bado unaitwa Ukristo, lakini hauna ukakamavu na nguvu kubwa.

Na nilikuwa Rome na kufanya mazungumzo na Papa juu ya suala hili na nafikiri mtakubaliana na hilo – kwamba maisha halisi ya Ukristo hivi sasa yako kule tunakokuita ulimwengu wa tatu,” amesema.