Mfumo wa afya nchini Haiti unakaribia kuporomoka-UNICEF

Waandamanaji wakichoma moto matairli huko Port-au-Prince Machi 12, 2024. Picha na AFP

Mfumo wa afya nchini Haiti unakaribia kuporomoka, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limeonya katika taarifa yake wiki hii.

Mchanganyiko wa vurugu, kuhama kwa watu wengi, magonjwa hatari na kuongezeka kwa utapiamlo, kumeathiri mfumo wa afya wa Haiti, alisema Bruno Maes, mwakilishi wa UNICEF nchini Haiti. Lakini upangaji wa mzunguko wa usambazaji unaweza kuwa ndio inaouvunja.

UNICEF imesema hospitali sita kati ya 10 nchini Haiti haziwezi kufanya kazi kwa sababu ya ghasia katika mji mkuu wa nchi hiyo, Port-Au-Prince.

Kuongezeka kwa ghasia hizo kunawanyima watoto dawa za kuokoa maisha pamoja na vifaa vya afya, kulingana na UNICEF.

Taarifa ya UNICEF inakuja wakati polisi wa Kenya hivi karibuni wanatarajiwa kuanza operesheni ya kimataifa inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa nchini Haiti, inayolenga kukabiliana na ghasia za magenge.

UNICEF imesema inatumia njia nyingine za usafirishaji ili kuwapatia watoto wa Haiti dawa na chanjo zinazohitajika.

Haiti iliripoti visa 82,000 vya ugonjwa wa kipindupindu kati ya Oktoba 2022 na Aprili 2024. Takriban watu milioni 4.4 nchini humo wanahitaji msaada wa dharura wa chakula.

UNICEF imeonya kuwa upatikanaji duni wa chakula unaongeza hatari ya kupoteza watoto kutokana na utapiamlo.