Mfanyakazi wa zamani wa VOA ajiua Iran

  • VOA News

Mfanyakazi wa zamani wa VOA Idhaa ya Uajemi, Kianush Sanjari, aliyejiuwa Alhamisi mjini Tehran

Idhaa ya Uajemi ya Sauti ya Amerika Alhamisi imeelezea kushtushwa na pia kuomboleza kufuatia kujiua kwa mmoja wa wafanyakazi wao  wa zamani ambaye aliruka kutoka kwa jumba la ghorofa mjini Tehran, kama ishara ya kupinga utawala kandamizi wa Iran.

Sanjari mwenye asili ya Iran na ambaye ana umri wa miaka 42 alikuwa mwanahabari na mwanaharakati wa haki za binadamu, aliyefanya kazi VOA, Idhaa ya Uajemi hapa Washington DC, kwa miaka kadhaa mwishoni mwa miaka ya 2000 na mapema 2010 kabla ya kurejea Iran 2016, ili kuwa karibu na wazazi wake.

Sanjari aliwahi kufungwa jela huko Iran kutokana na uanaharakati wake, na baada ya kuacha kufanya kazi Marekani, alizungumza wazi wazi kuhusu alivyoathirika kimawazo kutokana na kufungwa jela, pamoja na kuteswa na serikali ya Iran.

Mkuu wa Idhaa ya VOA Uajemi Leili Soltani, aliandika kwenye Instagram kwamba yeye na wafanyakazi wengine wameghadhabishwa na kuvunjwa moyo, kutokana na kifo cha mwenzao. “Kifo hicho ni pigo kubwa na chenye kutisha kwa kila mmoja aliyefanya kazi naye kwenye idhaa vya VOA Uajemi,” Soltani aliandika.

Mkuu wa VOA Michael Abramowitz pia alielezea kusikitishwa kwake na kifo cha Sanjari.