Mfalme wa Uingereza Charles amelihutubia bunge la Uingereza kwa mara ya kwanza kama kiongozi wa ufalme.
Alitoa hotuba yake katika ukumbi wa Westiminster uliopo jijini London mbele ya umma wa watu 1,000 ukijumuisha wabunge na wageni wao baada ya wabunge kutoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha mama yake aliyekuwa malkia wa Uingereza, Elizabeth.
Mfalme Charles na mkewe Camilla, Malkia wa Consort wanasafiri kwenda Edinburg leo hii ambapo mfalme atajiunga na ndugu zake kuendelea na shughuli nyingine za mazishi ambapo jeneza lenye mwili wa mama yake utapelekwa kwenye kasri la Holyroodhouse makazi maalumu ya ufalme wa Uingereza ya Scotland kwenda kanisa la mtakatifu Giles.
Mwili wa malkia Elizabeth utawekwa katika kanisa ambapo umma utaruhusiwa kutoa heshima za mwisho.