Meli ya kivita ya Marekani inayotumia nyuklia imewasili Jumamosi nchini Korea Kusini kwa mazoezi ya pande tatu ikiongeza mafunzo yao ya kijeshi katika kukabiliana na vitisho vya Korea Kaskazini ambavyo viliongezeka kwa ushirikiano wake na Russia.
Kuwasili kwa USS Theodore Roosevelt huko Busan kumekuja siku moja baada ya Korea Kusini kumuita haraka balozi wa Russia kupinga makubaliano yaliyofikiwa kati ya Rais wa Russia Vladimir Putin na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, wiki hii ambayo yanaahidi msaada wa ulinzi wa pamoja katika tukio la vita.
Korea Kusini inasema makubaliano hayo ni tishio kwa usalama wake na kuonya kuwa inaweza kufikiria kutuma silaha kwa Ukraine kusaidia kupambana na uvamizi wa Russia kama jibu, hatua ambayo bila shaka itaharibu uhusiano wake na Moscow.