Mchakato wa kutafuta katiba mpya umeshika kasi Tanzania

Waandamanaji wanaotaka katiba mpya wakiwa jijini Dar-es-salaam Tanzania, katika mojawapo ya maandamano ya kuishnikiza serikali kuandika katiba mpya

Wizara ya Katiba na Sheria nchini Tanzania imesema kwamba suala la kuanza mchakato wa kupata katiba mpya nchini humo ni moja ya vipaumbele vyake kwa mwaka huu ikisisitiza zaidi utoaji wa elimu kwa wananchi wa namna ya kupata katiba bora

Akizungumza jijini Dar-es-salaam waziri wa katiba na sheria Dkt Damas Ndumbaro amesema kuwa mara nyingi masuala ya katiba yanazungumzwa zaidi na wanasiasa lakini sasa wanataka kuhusisha wananchi kwa kiwango kikubwa ili kuweza kupata katiba itakayotosheleza matakwa ya wananchi.

“mjadala uliopo sasa hivi kwamba tupate katiba ya tano. Ndio mjadala uliopo mezani. Sisi tunataka katiba ambayo ni nzuri zaidi ili tusije tena baada ya muda mfupi tukajikuta tunatengeneza katiba ya sita. Katiba siyo sheria kwamba utakwenda bungeni unatunga na yanaisha, katiba ndio kila kitu katika jamii. “amesema Dkt Damas, akiongezea kwamba “Kwa sisi Tanzania ni vizuri zaidi tufahamu kwamba pamoja na mambo mengine, katiba hii imebeba mambo ya muungano na muungano wetu huu ni tunu. Muungano ni kitu kingine kabisa.”

Amesema kwa kushirikiana na asasi zisizo za kiserikali wizara ya katiba na sheria inatarajia kuanza mchakato wa kutoa elimu hiyo kwa wananchi kuhusiana na mambo yanayopatikana ndani ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ili kuwajengea uelewa wa kutambua masuala ya katiba na sheria

Maamuzi ya Chama cha CCM kuhusu katiba mpya

Suala la upatikanaji wa katiba mpya nchini Tanzania liliingia katika mkwamo kwa kipindi kirefu lakini katika siku za hivi karibuni suala hilo limepata msukumo mpya hususan baada ya vikao vya juu vya chama tawala CCM chini ya mwenyekiti wake wa Taifa ambaye pia ni Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kutoa tamko la kuishauri serikali kuangalia namna bora ya Kufufua, kukwamua na kuendeleza mchakato wa Katiba Mpya kwa kuzingatia mazingira ya sasa kwa maslahi ya Taifa.

Tangazo hilo lilitolewa baada ya vikao vya Kamati Kuu na Halmashashauri Kuu Taifa, uliofanyika Dodoma, Juni 21 na 22, 2022.

Mchakato wa kupatikana katiba mpya Tanzania ulikwama mwaka 2014 na umefufuliwa ili kupata katiba itakayochukua nafasi ya iliyopo kwa sasa, iliyotungwa mwaka 1977.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Shaka Hamdu Shaka akitangaza msimamo wa chama kinachotawala, alisema kwamba “CCM imeona umuhimu wa Katiba Mpya kwa mazingira ya sasa Tanzania, Serikali inaagizwa kuratibu ufufuaji wa mchakato wenyewe ikiwemo kuukwamua toka kwenye mkwamo kwa lengo la kukamilisha mchakato hadi kupata Katiba mpya na kwamba mchakato huo unafanywa kwa kuzingatia maslahi mapana ya taifa.”

Maswala makuu yanayozungumziwa katika katiba mpya ya Tanzania

Wanaotaka katiba mpya Tanzania wanasema kwamba katiba ya sasa iliyoandikwa mwaka 1977, imepitwa na wakati na haikidhi mazingira ya sasa ya Tanzania wakisema kuna migawanyiko ya kisiasa na kiuchumi.

  • Wanataka mammlaka ya rais kupunguzwa
  • Wanataka kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi
  • Kuwepo uwazi katika uteuzi wa majaji na wala sio kuwa jukumu la rais pekee
  • Ugawaji wa rasilimali kwa usawa. Sehemu nyingine za nchi zimeendelea sana kuliko nyingine

Mchakato wa kupata katiba mpya ulianzishwa wakati wa utawala wa Jakaya Kikwete

Aliyekuwa rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete aliwatangazia watanzania kwamba serikali yake ilikuwa na nia ya dhati ya kuandika katiba mpya, katika hotuba yake kwa umma siku ya mkesha wa kuufunga mwaka 2010

Mjadala mkali ulijitokeza baada ya tangazo la rais, ndani na nje ya chama chake, na kuashiria kwamba huenda hapakuwa na ridhaa ya chama chake cha mapinduzi CCM, kabla ya kutoa tangazo hilo.

Rasimu ya Mswaada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Na. 8 wa Mwaka 2011 ilitolewa Machi 31 na baadaye ikafuatiwa na kuunda tume ya Mabadiliko ya Katiba mwezi Aprili mwaka huo, kabla ya kukwama mwaka 2014.

Hatua zinazofuatwa kwa sasa

Katika mpangilio wa sasa, mchakato wa kuandika katiba mpya umeanzia ndani ya chama cha mapinduzi CCM na kuatangazwa na afisa wa ngazi ya juu wa chama hicho, baada ya maamuzi ya chama.

Serikali imeonekana kuanza kuwashawishi wanachama wa CCM katika ngazi zote na raia kutakiwa kujihusisha zaidi katika mchakato huo, pamoja na kupata msaada wa asasi za kiraia. Wanasiasa wa upinzani na viongozi wa kidini wamesikika wakiunga mkono hatua ya kuandika katiba mpya ya Tanzania.

“Tangu mheshimiwa rais wa awamu ya sita ameingia madarakani. Amesisitiza sana ushirikiano na asasi za kiraia. Alihudhuria maadhimisho ya miaka 10 ya watetezi wa haki za binadamu Tanzania akiwa mgeni rasmi na ni rais wa kwanza barani Afrika kufanya kitu kama hicho. Na sisi wizara tumefanya hivyo. Tunashirikiana sana na asasi za kiraia. Tumefanya mikutano na asasi za kiraia kuongelea haki za kibinadamu. Tumetengeneza mchakato wa kushirikiana nao lakini tumesema tutatoa tangazo kuzialika zile asasi za kiraia zinazotaka kutoa elimu ya katiba zilete maombi ndani ya mwaka huu wa fedha ambao unaanza tarehe moja Julai hadi 30. Zitakazoleta, tutawapa kazi ya kwenda kufundisha. Kwenye kufundisha, tunataka watuambie vitu viwili tu – uzuri na ubaya wa katiba hii.” Amesema waziri wa katiba na sheria Dkt Damas Ndumbaro.

Mchango wa bunge la Tanzania

Sheria ya kuandika Katiba mpya ilipitishwa na bunge Novemba 2011. Marekebisho kwenye sheria hiyo yalikamilika mwaka 2014.

Sheria hiyo iliweka utaratibu wa kisheria kuruhusu mchakato huo kuendelea.

Mchakato wa awali ulikwama baada ya rasimu kuasilishwa kwa rais kwa uzinduzi rasmi badala ya kupelekwa bungeni.

Wanasheria walisema ilikuwa ni makosa kwa rais kufanya hivyo.

Kura ya maoni

Baada ya rasimu ya katiba mpya kuandikwa, itafanyiwa kura ya maoni ili watanzania wote wawe na uwezo wa kuamua hatma ya nchi yao.

Hii ni hatua ya mwisho kwa mchakato huo iwapo asilimia 50 ya wapiga kura wataikubali na utaratibu wa utekelezaji wa Katiba hiyo mpya utaanza mara moja.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA Washington DC na Dinah Chahali, Dar-es-salaam