Mchakato wa BBI wa kutaka kuifanyia marekebisho katiba ya Kenya si halali - Mahakama Kuu

Jaji wa mahakama kuu ya Kenya, George Odunga.

Mahakama Kuu ya Kenya, Alhamisi usiku iliamuru kwamba mchakato uliokuwa ukiendelea wenye nia ya kuifanyia marekebisho katiba ya nchi hiyo ya mwaka wa 2010, si halali.

Majaji watano waliokuwa wakisikiliza hoja tisa za kupinga kwendelea kwa mchakato huo, walikubaliana kwa kauli moja kwamba kamati ya BBI iliyoundwa na Rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa hasimu wake wa kisiasa Raila Odinga ilikiuka sheria na katiba ya nchi hiyo.

Aidha, jopo hilo lilifikia makubaliano kwamba rais wa Kenya hana uwezo wa kikatiba wa kuanzisha mchakato wa kutaka kufanya marekebisho ya katiba ya nchi hiyo.

Majaji hao, Prof Joel Ngugi, George Odunga, Jairus Ngaah, Teresia Matheka na Chacha Mwita, walisema kwamba mchakato huo unakiuka kipengele cha 257 cha katiba ya mwaka wa 2010.

"Ni jukumu la bunge kuanzisha mchakato kama huo na wala sio rais," alisema mmoja wa majaji hao.

Ailiongeza kwamba rais anaweza kufunguliwa mashtaka kama raia, hata akiwa madarakani, iwapo atakiuka katiba.

Uamuzi huo, uliogusia masuala mbalimbali, uslisomwa na majaji kadhaa mmoja kwa mmoja.

Jaji Ngugi, mwenyekiti wa jopo hilo alisema: "Ni kinyume cha katiba kwa mswada wa bunge kupendekeza ongezeko la idadi ya majimbo au maeneo wakilishi wa bunge."

"Rais Uhuru Kenyatta amekiuka sheria kwa kuanzisha au kuzindua mchakato wa kutaka kuifanyia marekebisho ya katiba," uamuzi huo ulieleza.

Mahakama hiyo pia iliamuru kwamba tume ya uchaguzi na mipaka IEBC, haiwezi kushiriki kwenye mchakato wa kuifanyia katiba marekebisho, kwa sababu imekiuka katiba na sheria kwa sababu haijakuwa ikiendelea na mchakato wa mfululizo wa kuwasajili wapiga kura.

Aidha, jopo hilo lilisema mchakato huo ulikiuka katiba kwa sababu haukuwashirikisha raia moja kwa moja.

Mahakama hiyo ilikuwa ikisikiliza hoja tisa zilizokuwa zimejumulishwa pamoja, zilizo wasilishwa na wadau mbalimbali.

Walikuwa wamewashtaki mwanasheria mkuu wa Kenya, Kihara Kariuki, Spika wa Baraza la wawakilishi Justin Muturi na mwanzake wa baraza la Seneti Ken Lusaka, pamoja na Tume ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC.

Baadhi ya hoja zilizosikilizwa zilikuwa zimewasilishwa na mwanaharakati na mchumi David Ndii, na raia wengine wa Kenya Jerotich Seii, James Ngondi, Wanjiku Gikonyo and Ikal Angelei.

Hata hivyo, hoja iliyopinga mchakato wa kufanya kura ya maoni kwa sababu ingehatarisha maisha ya Wakenya wakati wa janga la Covid-19, ilikataliwa na mahakama.

Haya yalijiri siku chache baada ya mabunge mawili - lile la kitaifa na lile la Seneti - kupitisha miswada ya marekebiso ya katiba katika mchakato ulioibua joto kubwa la kisiasa.

Punde tu baada ya uamuzi huo wa mahakama, naibu wa Rais wa Kenya, William Ruto, bila maelezo zidi, alituma ujumbe kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter uliosema, "Kuna Mungu mbinguni. Kwa kweli Mungu anaipenda Kenya,"

Ingawaje wadau wana uhuru wa kukata rufaa, wachambuzi wanasema uamuzi wa Alhamisi huenda ukaathiri kwa kiasi kikubwa uwezekano wa kufanyika kwa kura ya maamuzi kabla ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka ujao.

"Hakuna muda wa kutosha wa kushugulikia rufaa ya kesi hiyo kabla ya uchaguzi wa mwaka ujao. Ningeshauri watulie tu," alisema wakili Elias Mutuma, akizungumza na kituo cha televisheni cha Citizen mjini Nairobi.

Alhamisi jioni, vyombo vya habari mjini Nairobi viliripoti kwamba mwanasheria mkuu wa Kenya Kihara Kariuki aliashiria kwamba angakata rufaa, na kuiomba mahakama kumpa nakala kamili ya uamuzi wake.