Mbunge-Tanzania aondoa pendekezo la ukomo wa ubunge

Jengo la Bunge la Tanzania

MBUNGE wa Chemba kwa tiketi ya chama tawala CCM, nchini Tanzania Juma Nkamia, ameondoa kwa muda kusudio lake la kutaka kuwasilisha muswada binafsi wa mabadiliko ya Katiba ya nchi ili kuongeza ukomo wa ubunge kutoka mitano hadi saba.

Nkamia aliwasilisha kusudio hilo Septemba, mwaka huu mjini Dodoma kwa mujibu wa kanuni ya 81(2) ya kanuni za Bunge toleo la 2016, kupitia barua yake aliyoisaini Septemba 12, mwaka 2017.

Kupitia ujumbe mfupi aliouandika katika mtandao wa kijamii wa WhatsApp, Nkamia alisema ameamua kuondoa kusudio hilo baada ya majadiliano na maelekezo kutoka kwa viongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Ndugu viongozi wenzangu, naomba kuwataarifu kuwa baada ya mashauriano na maelekezo ya viongozi wa juu wa CCM na hali ya kisiasa katika nchi kadhaa za Afrika Mashariki, nimelazimika kuondoa kwa muda hoja yangu binafsi ya ukomo wa Bunge niliyokusudia kuiwasilisha katika Bunge lijalo (linaloanza Novemba, mwaka huu,” ujumbe huo ulieleza.

Aliongeza kuwa : “Naomba ibaki hivyo hivyo kama ilivyo kwenye meseji sina cha kuongeza, kuhusu ni lini nitapeleka tena nayo subiri kwa sababu nimesema nimesitisha kwa muda, maana yake nitawasilisha tena nitakapokuwa tayari.”

Hoja ya Nkamia ilianzia Bunge lililopita lakini ilipingwa na wanasiasa wakongwe akiwamo Spika Mstaafu wa Bunge, Pius Msekwa na wasomi mbalimbali.

Akizungumza na Kituo cha Televisheni cha Azam, Alhamisi wiki iliyopita, Spika wa zamani wa Bunge la Muungano, Pius Msekwa alisema CCM haiwezi kukubaliana na maoni ya kuongeza muda wa kiongozi yeyote kutoka kipindi cha miaka mitano kilichopo kwa mujibu wa Katiba ya sasa.

Pia alisema kwa uzoefu wake bungeni anaona kuna tafakuri nyingi zilizofanywa kabla ya Taifa kuamua kipindi cha utawala kuwa miaka mitano na si vinginevyo.