Mbunge kutoka chama kidogo ashinda uchaguzi wa rais nchini Sri Lanka

  • VOA News

Mbunge aliyeshinda uchaguzi wa rais Anura Kumara Dissanayake. Picha ya AP

Mbunge wa siasa za Kimarxist nchini Sri Lanka, Anura Kumar Dissanayake alishinda uchaguzi wa rais kwa ahadi za kuwasaidia watu maskini na kutokomeza ufisadi katika nchi hiyo ambako mdororo wa uchumi miaka miwili iliyopita ulisababisha shinikizo la mabadiliko makubwa.

Ushindi huo unaonyesha mabadiliko makubwa katika siasa za nchi hiyo ya Kusini mwa Asia, ambayo imepinga vyama vikuu vya kisiasa ambavyo vimetawala nchi hiyo kwa miongo kadhaa.

Dissanayake mwenye umri wa miaka 55, anayejulikana kwa msimamo wake wa kuunga mkono wafanyakazi, anaongoza muungano wa vyama vya mrengo wa kushoto, the National People’s Power.

Chama chake, JVP, ambacho wakati mmoja kilikuwa na msimamo mkali, kina viti vitatu tu katika bunge lenye wabunge 225 na haikajawahi kuwa miongoni mwa vyama vikuu.

“Ushindi huu ni wetu sote”, Dissanayake aliandika kwenye mtandao wa X. “ Tuko tayari kuandika upya historia ya Sri Lanka.”