Mazunguzo ya nyuklia ya Iran kuanza tena

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Ned Price

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Ned Price Jumatano amedhibitisha kwamba duru ya 7 ya mazungumzo ya nyuklia ya Iran itaanza Novemba 29 mjini Vienna, Austria.

Price amesema kwamba mazungumzo hayo yatahusisha Iran na mataifa yaliobaki kwenye mkataba, wakati Marekani ikishiriki kama mgeni kupitia Robert Malley ambaye ni mjumbe maalum wa Marekani kwenye masuala ya Iran, anayeongoza ujumbe wa Marekani.

Price ameongeza kusema kwamba iwapo mazungumzo hayo yanatarajiwa kufaulu, basi ni sharti yaanzie pale ambapo mazungumzo ya 6 yalipomalizikia. Mjumbe maalum wa EU Enrique Mora amekuwa akiongoza mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Marekani na Iran pamoja na wanadiplomasia kutoka EU, Russia na China miongoni mwa mataifa mengine yalioko kwenye mkataba.

Mazungumzo hayo yanalenga kufufua mkataba wa 2015 kati ya mataifa hayo na Iran ya kusitisha program ya nyuklia. Rais wa Marekani aliyeondoka madarakani Donald Trump mwaka wa 2018 aliondoa Marekani kwenye mkataba huo wakati akiongeza vikwazo kwa Iran.