Trump Ataridhia Makubaliano Yoyote Kati ya Israel na Palestina

Rais Donald Trump (kulia) akisalimiana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

Rais Donald Trump amesema Jumatano kuwa makubaliano ya amani kati ya Israel na Palestina huenda yasihusishe kuundwa kwa taifa huru la Palestina.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari akiwa na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, Trump amesema Jumatano yeye atapendelea makubaliano yoyote yatakayofikiwa na pande hizo mbili kupitia mazungumzo ya moja kwa moja.

“Mimi natarajia makubaliano ya kuwepo mataifa mawili au taifa moja,” amesema Trump. “Nitaridhia kile ambacho wao watakipendelea.”

Trump ameisihi Israel “isitishe” ujenzi wa makazi mapya ya Israel, na kusema Wapalestina waache kuwafundisha vijana wao kuichukia Israel.

Afisa wa ngazi ya juu wa White House ameeleza kubadilika kwa sera ya Marekani kuhusu mgogoro wa Israel na Palestina wakati akizungumza na waandishi Jumanne.

Amesema kuwa kupatikana kwa amani kati ya Waisraeli na Wapalestina siyo lazima iwe kupitia suluhisho la mataifa mawili, na ni juu ya pande hizo mbili kuamua.

Afisa huyo amesema kuwa Marekani “haitatoa masharti yoyote katika kufikia amani.”

“Suluhisho la kuwa na mataifa mawili ambalo halitaleta amani sio lengo ambalo mtu yoyote anataka kulifikia,” afisa huyo amesema.

Amani ndio lengo, haijalishi kama itapatikana katika njia ya suluhisho la kuwa na mataifa mawili ikiwa tu pande mbili hizo zinataka hilo au ikiwa ni utaratibu mwingine kama wenyewe wamekubaliana. Sisi tuko tayari kuwasaidia.”