Mwili wake Annan umewekwa kwenye ukumbi wa mikutano ya kimataifa mjini Accra ambapo ibada ya kumuaga inafanyika kabla ya kuzikwa Alhamisi.
Wageni waheshimiwa kutoka kote duniani wanahudhuria mazishi ya kiongozi huyo. Kati yao akiwemo Katibu Mkuu wa UN wa sasa Antonio Gutterrez na Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast.
Vyombo vya habari nchini Ghana vinaeleza kwamba baadhi ya waombolezaji hawakuridhishwa na hatua ya jeneza la Annan kufunikwa na kuwazuia waombolezaji kumuona kwa mara ya mwisho kiongozi huyo wa zamani.
Mjane wa aliyekuwa Rais wa kwanza Afrika Kusini Nelson Mandela - Graca Machel na Gro Harlem Brundtland ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu nchini Norway ni miongoni mwa wanaohudhuria mazishi ya Annan.
Kwa mujibu wa ratiba ya mazishi yake sehemu ya shughuli zinajumuisha maafisa kutoa heshima zao kwa jamaa na familia ya Annan.
Annan, ni kiongozi wa pili wa Afrika kushikilia nafasi ya juu ya UN kama Katibu Mkuu.Annan aliaga duniai mwezi Agosti akiwa nchini Uswizi na umri wa miaka 80.