Dunia yaadhimisha siku ya wafanyakazi

  • Mkamiti Kibayasi

Rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia katika sherehe za siku ya wafanyakazi Duniani zlizofanyika kitaifa mkoani Tanga

Wito wa nyongeza ya mishahara, mfumuko wa bei na mazingira bora ya kazi ni moja ya malalamiko yanayoelezwa na kila mfanyakazi duniani katika siku ya Mei Mosi

Maelfu ya wafanyakazi duniani kote wanaandamana mitaani katika miji mbali mbali kuadhimisha siku ya kimataifa ya wafanyakazi - Mei Mosi - ambapo wanatoa wito wa nyongeza ya mishahara na mazingira bora ya kufanyia kazi.

Nchini Tanzania Rais Jakaya Kikwete alikuwa mgeni rasmi katika sherehe zilizofanyika kitaifa katika mkoa wa Tanga ambapo wafanyakazi wa mji huo walikuwa na malalamiko sambamba na yale yanayozungumziwa na wafanyakazi wengine sehemu mbali mbali duniani.

Jijini Dar Es Salaam wafanyakazi waliungana na kaimu mkuu wa mkoa huo Mwantumu Maiza kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja kuadhimisha sherehe hizi kimkoa ambapo wafanyakazi walishika mabango yanayoelezea “tunasema kodi kubwa, mishahara kidogo ni mzigo kwa wafanyakazi”

Wakati huo huo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dr. Ali Mohamed Shein alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizi visiwani humo. Wafanyakazi wa Zanzibar walipita na mabango mbele ya Rais yanayosomeka kuwa “Utawala bora ni pamoja na ushirikishwaji wa wafanyakazi kwa maendeleo ya nchi. Pia kuna ujumbe mwingine uliosomeka “mfumuko wa bei, kodi kubwa na mishahara duni ni pigo kwa wafanyakazi.

Huko Asia maelfu ya wafanyakazi walikusanyika katika miji mikuu ya Thailand, Bangladesh na Indonesia kuadhimisha siku hii kwa kufanya maandamano yaliyoandaliwa na vyama vya wafanyakazi. Shirika la habari la Ufaransa linasema maandamano mjini Jakarta yalikuwa makubwa sana kufanyika kwa bara hilo.