Taarifa iliyotolewa Jumatatu na makao makuu ya waziri mkuu, 10 Downing Street, imesema kuwa Bi May alikuwa amepokea barua ya kujiuzulu kwa waziri Johnson na kumsifu kwa utendakazi wake.
Taarifa hiyo iliongeza kwamba mtu atakaye chukua nafasi ya waziri huyo wa zamani atatangazwa muda si mrefu.
Mapema Jumatatu, waziri David Davis wa masuala ya Brexit alikuwa amekiambia kituo cha utangazaji cha BBC kwamba Uingereza haidai haki yake katika mchakato huo wa kujiondoa kutoka katika muungano huo wa umoja wa ulaya (EU).
"Tunapeana mengi sana katika mchakato huu wa Brexit," alisema Davis.
CNN iliripoti Jumatatu kwamba kujiuzulu kwa mawaziri hao ni pigo kubwa kwa waziri mkuu Theresa May na mstakabali wake kisiasa.
Muda mfupi baada ya kujiuzulu kwa Johnson, May alilihutubia bunge la nchi hiyo na kutetea hatua anazozichukua katika mchakato mzima wa Brexit.
Pamoja na kuwa mwanasiasa, Johnson ambaye alizaliwa mwaka wa 1964, ni mwanahistoria na mwandishi wa habari. Amewahi kuwa mbunge tangu mwaka wa 2001 hadi 2008, na meya wa mji wa London kutoka mwaka wa 2008 hadi 2016.
Johnson ambaye anaegemea siasa za mrengo wa kiafidhina, mara kwa mara hujitambulisha kama mtu anayeunga mkono sera za kuiunganisha Uingereza haku akitetea sera za uchumi huru.
Johnson, aliyezaliwa mjini New York, Marekani, amekuwa mmoja wa wanasiasa tajika nchini Uingereza, ambaye aliunga mkono kampeni ya kujiondoa kwa Uingeereza kutoka kwa Umaoja wa ulaya.
Lakini katika siku za karibuni, amekuwa akionekana kama ambaye haungi mkono baadhi ya misimamo ya waziri mkuu May kuhusu mchakatio huo wa kujitoa kwa European Union.
David Davis, ambaye alijiuzulu Jumapili, aliteuliwa kuratibu masuala ya kujiondoa kwa Uingereza baada ya waziri mkuu May kuunda wizara hiyo mnamo mwaka wa 2016 kufuatia kura ya maoni ambapo Waingereza wengi walitaka nchi yao iondoke kwa uanachama wa muungano huo.
Kabla ya hapo alikuwa mbunge wa eneo wakilishi la Haltemprice and Howden tangu mwaka wa 1997.
Katika siku za karibuni, Davis amekiri kwamba mazungumzo kuhusu mchakato wa Brexit yamekuwa magumu.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaeleza kwamba hawakutarajia kwamba mawaziri hao wangejiuzulu kwa siku moja.