Mawaziri wa Ufaransa na Ujerumani wafika Ethiopia

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed

Mawaziri wa mambo ya nje wa Ufaransa na Ujerumani wamewasili nchini Ethiopia kuunga mkono makubaliano ya amani ya mwezi Novemba kati ya serekali ya shirikisho na Tigray ya kumaliza miaka miwili ya vita vya kikatili. 

Mawaziri wa mambo ya nje wa Ufaransa na Ujerumani, Catherine Colonna na Annalena Baerbock, walikutana Alhamisi na Waziri Mkuu Abiy Ahmed, katika ziara ya kuunga mkono makubaliano ya amani ya Tigray.

Makubaliano hayo ya Novemba yameshuhudia maendeleo makubwa huku huduma za msingi zikirejeshwa katika eneo la Tigray, kuongezeka kwa misaada, na makabidhiano ya kwanza ya silaha na chama cha Tigray People’s Liberation Front na vikosi vya shirikisho vya Ethiopia.

Mashuhuda wanasema wanajeshi wa Eritrea, mwezi Disemba waliondoka katika miji miwili ya Tigray lakini bado haijabainika ikiwa wanakusudia kuondoka kabisa katika eneo hilo.

Viongozi hao wa Ulaya pia watakutana na maafisa wa Umoja wa Afrika kwenye makao yake makuu Addis Ababa.

AU ulisimamia makubaliano ya amani ya Tigray na waangalizi wake walifika katika mkoa huo mwezi huu kusimamia utekelezaji wake.

Ufaransa na Ujerumani pia zinataka kusaidia uhaba wa chakula unaosababishwa na ukame uliolikumba eneo la Pembe ya Afrika na kutatiza usambazaji wa nafaka na kuongezeka kwa bei yz vyakula kutokana na vita vya Russia na Ukraine.

Ziara hiyo ya siku mbili inajumuisha kutembelea ghala za shirika la Mpango wa Chakula Duniani katika mkoa wa Oromia, ambako ngano iliyotolewa kutoka Ukraine ili kusaidia kukabiliana na njaa inahifadhiwa.

Serikali za Ufaransa na Ujerumani zilifadhili usambazaji wa nafaka zinazohitajika sana na zinatarajiwa kutangaza msaada mpya kwa watu katika maeneo yaliyoathiriwa na vita vya miaka miwili vya wenyewe kwa wenyewe nchini Ethiopia.

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wanasema kuna ushahidi wa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu unaofanywa na pande zote katika mzozo huo, ikiwa ni pamoja na ubakaji, mateso, na mauaji holela.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa mwezi Septemba ilisema serikali ya Ethiopia na washirika wake pia walitumia njaa kama silaha ya vita, jambo ambalo wanakanusha.

Umoja wa Mataifa unasema mamilioni ya watu walikimbia makazi yao katika vita hivyo na zaidi ya Watigray milioni tano wanahitaji msaada wa kibinadamu.