Mawaziri wa fedha na wakuu wa benki kuu kutoka kundi la nchi 20 tajiri wanakutana uso kwa uso Ijumaa huko Venice nchini Italy kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa janga la COVID-19 ambapo mageuzi ya kodi za makampuni itakuwa ajenda kuu.
G-20 inatarajiwa kutoa idhini yake ya kisiasa kwa kanuni mpya juu ya wapi na kiasi gani kampuni zitatozwa kodi hatua ambayo iliungwa mkono wiki iliyopita na nchi 130 kwenye taasisi ya maendeleo na ushirikiano wa kiuchumi yenye makao yake Paris.
Mpango huo unafikiria kuweka kiwango cha chini cha kodi ya mapato ya kampuni kwa angalau asilimia 15 kiwango ambacho OECD inakadiria kinaweza kupata takribani dola bilioni 150 katika mapato ya ziada ya kodi ulimwenguni lakini bado maelezo mengi hayajazungumziwa.