Mamlaka ya mawasiliano ya Mauritius imeamuru kufungwa kwa mitandao yote ya kijamii nchini humo kuanzia leo Ijumaa Novemba Mosi hadi Novemba 11 siku moja baada ya uchaguzi mkuu.
Hatua hiyo imechukuliwa wakati nchi inakabiliwa na kashfa za mawasiliano ya watu maarufu kunaswa na kuwekwa wazi kwenye mitandao ya kijamii.
Waandishi wa habari wasiokuwa na mipaka wamesema mawasiliano ya watu 20 wakiwemo wanasiasa, polisi, mawakili, waandishi wa habari, na wanachama wa mashirika ya kijamii yamenaswa na kuwekwa kwenye mitandao ya kijamii tangu katikati mwa mwezi Oktoba.
Mamlaka ya mawasiliano imesema hatua ya kufunga mitando ya kijamii inatokana na mawasiliano ya watu kusambazwa kwenye mitandao hiyo, ambapo mamlaka inasema ni kinyume cha sheria.
Ofisi ya Waziri Mkuu imesema kwamba hatua ya kufunga mitandao ya kijamii ni muhimu kwa ajili ya usalama wa taifa na heshima ya taifa.