Nchi za Afrika hasa zilizokuwa koloni la Ufaransa ziliendelea kutalakiana na Ufaransa, zikisitisha ushirikiano wa kijeshi huku maandamano yakishuhudiwa katika nchi kadhaa.
Mojawapo ya matukio yalitogonga vichwa vya habari Afrika mwaka 2024 ni siasa za Afrika kusini ambapo chama kinachotawala cha the African National Congress (ANC) kilishindwa kupata idadi ya kutosha ya viti vya bunge kuunda serikali pasipo msaada wa chama cha upinzani.
Licha ya Cyril Ramaphosa kushikilia uongozi wa Afrika kusini, ilibidi ANC kutafuta msaada wa chama cha Democratic alliance na kuunda serikali ya muungano.
Maandamano ya vijana Kenya
Nchini Kenya maandamano yalipelekea rais William Ruto kuondoa mswada wa fedha, kuvunja baraza la mawaziri, kutekeleza mabadiliko kadhaa katika serikali na kuwateua wanasiasa wa upinzani kuwa mawaziri.
Waandamanaji walivamia bunge n ahata kuchoma sehemu ya bunge. Siasa za Kenya zilijaa chuki za kikabila kiasi kwamba naibu rais Righathi Gachagua alitimuliwa ofisini na bunge na licha ya kukimbilia mahakamani kuzuia hatua ya senate kuidhinisha kutimuliwa kwake, hakunusurika.
Prof Kithure kindiki aliteuliwa kuwa naibu rais. Matukio ya moto shuleni vile vile yaliripotiwa Kenya, tukio la kushutukiza zaidi ni la Watoto 21 kufariki katika tukio la moto lililoteketeza bweni la shule ya msingi ya Endarasha Katikati mwa Kenya.
Utekaji nyara Tanzania
Katika nchi Jirani ya Tanzania, matukio ya watu kutekwa nyara au kupotea katika mazingira yenye utata yaligubika nchi hiyo kubwa Afrika mashariki.
Mabalozi na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu walitaka serikali kuchukua hatua kumaliza utekeaji nara.
Vyombo vya habari vimepitia hali ngumu mwaka huu baadhi vikifungiwa kwa muda huku waandishi wakiwa na uoga wa kuandika habari huru na zisizoegemea upande mmoja.
Ali Mohamed Kibao, mwanasiasa wa upinzani alitekwa nyara, kuuawa na baadaye mwili wake ukapatikana na majeraha mabaya Pamoja na kumwagiwa kemikali.
Mapigano kati ya waasi na wanajeshi wa serikali DRC
Nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo mapigano yaliendelea mwaka huu.
Waasi wa M23 waliendela kupigana na wanajeshi wa serikali. Mazungumzo yaliendelea kusitisha vita bila mafanikio.
Angola, kwa niaba ya umoja wa Afrika, ilifikia makubaliano ya kusitisha vita ambayo yalikosa kuheshimiwa.
Marekani iliamuru Rwanda kuondoa wanajeshi na silaha zake mashariki mwa DRC lakini hakuna lililofanyika.
Mgogoro wa kidiplomasia kati ya Ethiopia na Somalia
Katika pembe ya Afrika, mgogoro uliendela kati ya Ethiopia na Somalia, baada ya Somaliland kuingia makubaliano na Ethiopia, kutumia sehemu ya Bahari yake kwa shughuli za kibiashara na ulinzi.
Somalia inashikilia kwamba Ethiopia inaingilia mipaka yake na kwamba Somaliland haina uwezo wa kuingia makubaliano au mikataba na nchi yoyote kwani Sonaliland sio nchi huru inayotambuliwa kimataifa.
Uchaguzi mkuu Ghana, Madagascar, Rwanda, Namibia
Uchaguzi ulifanyika Madagascar ambapo Andry Rajoelina alishinda mhula wa tatu madarakani japo kulikuwa na idadi ndogo ya wapiga kura baada ya wanasiasa wa upinzani kususia uchaguzi huo.
Nchini Ghana aliyekuwa rais John Mahama alirejea ofisini baada ya kupata asilimia 56.55 ya kura.
Nchini Rwanda Paul Kagame aliweka historia kwa kupata asilimia 99 ya kura na kuendelea kutawala nchi hiyo ndogo ya Afrika mashariki.
Nchini Botswana chama cha Botswana Democratic party kilipata pigo la kihistoria na kubanduliwa madarakani baada ya miongo sita.
Rais Mokgweetsi Masisi alikiri kushindwa vibaya na mgombea wa upinzani Duma Boko.
Ni uchaguzi ambao uliwashinda hata wachambuzi na wakusanyaji wa maoni kutabiri.
Historia iliandikwa Namibia na Afrika. Netumbo Nandi Ndaitwah, alichaguliwa rais mwanamke wa kwanza kuongoza Namibia. Alipata asilimia 57 ya kura.
Nchini Msumbiji chama cha Frelimo kilisalia madarakani na kuendeleza utawala wa miongo mitano huku upinzani ukidai kuwepo wizi wa kura.
Daniel Chapo alipata asilimia 70 ya kura na kuchukua usukani wa nchi kutoka kwa Filipe Nyusi na kuwa rais wa 5 wa Msumbiji.
Wafuasi wa Venancio Mondlane aliyemaliza katika nafasi ya pili waliandamana, kukabiliwa na polisi na vifo vya watu kadhaa kuripotiwa.
Mapigano Sahel, Sudan
Katika eneo la Sahel, migogoro iliendelea Niger, Burkinafaso, chad na kwingineko. Nchi zilisokuwa koloni la kifaransa ziliendelea kuvuruga uhusiano wake na Ufaransa na kutaka wanajeshi wa Ufaransa kuondoka.
Nchini Sudan mapigano yaliendelea kusababisha vifo na uharibifu wa mali. Mazungumzo ya kusitisha vita kati ya jeshi la serikali SAF na kikosi cha kijeshi cha dharura RSF yalikosa kufanikiwa.
Mashirika ya kutoa misaada yanasema vita hivyo vimesababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu duniani, maelfu ya watu wakiwa katika hatari ya ukosefu wa chakula.
Hadi sasa, umoja wa mataifa na mashirika mengine, wanasema zaidi ya watu 20,000 wameafariki kutokana na vita vya Sudan.