Matokeo ya uchaguzi yaanza kutangazwa Tanzania

Kubandikwa kwa matokeo hayo kunafanywa baada ya kazi ya kujumulisha matokeo ya kura na hatimaye kusainiwa na pande zote ikiwemo maafisa wa tume hiyo pamoja na mawakala wa vyama vya siasa.

Baadhi ya vituo vya kupigia kura vimeanza kuweka hadharani baadhi ya matokeo ya uchaguzi uliofanyika Jumatano, Tanzania, ambao ni wa sita kufanyika tangu taifa hilo lilipoanzisha mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992.

Kubandikwa kwa matokeo hayo kunafanywa baada ya kazi ya kujumulisha matokeo ya kura na hatimaye kusainiwa na pande zote ikiwemo maafisa wa tume hiyo pamoja na mawakala wa vyama vya siasa.

Ingawa kumekuwa na ishara kwa baadhi ya wafuasi wa vyama kushangilia lakini matokeo ya mwisho ikiwemo yale ya udiwani na ubunge huenda yakaanza kujulikana kuanzia Alhamisi mchana au jioni.

Matokeo ya udiwani yatawasilishwa katika ofisi za watendaji wa kata wakati yale ya ubunge na urais yatapelekwa katika ofisi za wakurugenzi ambao ndiyo wenye jukumu la kutoa matokeo ya mwisho ya wabunge wakati yale ya urais hupelekwa moja kwa moja katika ofisi ya tume ya taifa ya uchaguzi.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu, Semistocles Kaijage amesema kwamba kata nne zilishindwa kufanya uchaguzi wa ngazi ya madiwani kutokana na sababu kuu mbili.

Mosi kata tatu hazikufanya uchaguzi huu baada ya wagombea wake kufariki dunia huku kata moja uchaguzi huo imebidi uahirishwe baada ya kukosewa kwa karatasi za kupigia kura.

Mwenyekiti huyo amesema kata hizo zitafanya uchaguzi wake katika muda utakaotangazwa hapo baadaye.

“Hata hivyo tukumbuke kuwa katika kata hizo, uchaguzi wa wabunge umeendelea kama ulivyopangwa,” amesema Kaijage.

Kumekuwa na ripoti kuhusu kuwepo kwa baadhi ya kura bandia katika baadhi ya vituo na nyingi ya ripoti hizo zinasema kura hizo zilikamatwa katika jimbo la Kawe jijini Dar es salaam, Pangani, Tanga na Buhigwe huko Kigoma.

Hata hivyo, mwenyekiti huyo wa tume amesema ripoti hizo hajabainisha bayana ni vituo gani ambako kura hizo zilikamatwa na wala tume haijathibitisha kuhusu madai hayo akisema kwamba “Taarifa za madai hayo hazijawasilishwa rasmi kwenye tume ya taifa ya uchaguzi. Tume inawasihi wananchi kupuuza taarifa hizo ambazo sio rasmi na hazijathibitishwa.”

Katika tukio hilohilo la kuwepo kwa kura bandia, mgombea ubunge wa Chadema katika jimbo la Kawe, Halima Mdee ameachiwa na jeshi la polisi baada ya kushikiliwa kwa muda kutokana na tafrani iliyojitokeza kuhusiana na suala hilo.

Wafuasi wa chama hicho waliokuwepo katika moja ya kituo cha kupigia kura walidai kuwa baadhi ya watu wakiwa na kura hizo hali iliyosababisha kuwepo vuta nikuvute.

Kwa upande mwingine kuendelea kuminywa kwa mitandao ya mawasiliano kama vile internet iliyopungua kasi kumesababisha kilio kikubwa kwa mamia ya wananchi wanaosema wanashangazwa na kitendo hicho wanachodai kinajitokeza kwa mara ya kwanza katika historia ya kurejea kwa uchaguzi wa mfumo wa vyama vingi tangu mwaka 1995.

“Kwa kweli hatujatendewa haki. Kwa sababu mitandao yote kuanzia twitter, Instagram na whatsapp haifanyi kazi. Sisi mitandao tunaitumia sio kwa kupiga kura tu. Wengine tunaitumia kufanya biashara. Imetuumiza sana. huwa tunasikia yanatokea sehemu nyingine na sisi yametukuta.” Amesema mkaazi wa Dar-es-salaam.

Kumekuwa na shida ya kupata mawasiliano ya internet huku baadhi ya huduma kama whatsapp, you tube, twiter na mitandao mingine ikisitishwa kabisa. Hii ni mara ya kwanza kwa hali kama hiyo kushuhudiwa nchini Tanzania.

Imetayarishwa na mwandishi wetu wa Dar-es-salaam, George Njogopa.