Katika mahojiano na Idhaa ya Kiswahili VOA Dkt Elias Isaack Mashala wa Hospitali ya Mt Meru Arusha Tanzania ambaye alifuatana na wanafunzi hao amesema kuwa wote watatu wanaendelea vizuri baada ya operesheni zao kufanikiwa.
Alisema operesheni ya mwanafunzi Doreen ilichukua muda mrefu, kuanzia saa kumi na nusu na kuendelea mpaka saa tano usiku.
Dkt Mashala alisema operesheni ya mwanafunzi Sadia ilianza saa nne asubuhi mpaka saa kumi jioni . Naye Wilson alifanyiwa upasuaji ulioanza saa mbili asubuhi mpaka as nne, amesema Dr Mashala.
Daktari huyo amesema kuwa Wilson and Sadia wanaendelea vizuri pengine wiki ijayo wanaweza kuruhusiwa kutoka hospitali huku wakiendelea kupata matibabu ya mazoezi na marekebisho ya viungo.
Kwa Doreen ambaye anahitaji marekebisho zaidi ya kiufundi ya tiba kwa jeraha lake la mgongo bado atakuwa na muda fulani wa kukaa hospitali.
Wanafunzi hao walipata ajali ya bus la shule Mei 6, 2017 katika eneo la Karatu, Arusha, ambapo wenzao 32 walifariki duniani pamoja na waalimu wawili na dereva.
Kwa mujibu wa Dkt Mashala watoto hao walikuwa wamepata majeraha makubwa sana.
Your browser doesn’t support HTML5
“Doreen alikuwa na majeraha ya kwenye taya na mivunjiko mibaya sana na ute wake wamgongo ulikuwa umeumia katika eneo la kifua,” amesema.
“Doreen ameanza kukaa baada ya upasuaji. Yeye alifanyiwa upasuaji mara ya pili wa mgongo kuimarisha zile sehemu zilizokuwa zimevunjika katika ute wa mgongo,” amefafanua.
Alieleza kuwa Wilson aliumia mikono yote miwili ambayo ilikuwa imepata mivunjiko ya mifupa katika maeneo ya viwiko.
Naye Sadia, daktari amesema kuwa hakuwa na mivunjiko mibaya sana katika shingo, na hivyo haukuhitaji kufanyiwa upasuaji lakini mikono yote miwili ilikuwa imevunjika na ilifanyiwa upasuaji.
“Kwa ujumla jinsi walivyopata majeraha inaonekana walirushwa na kutua katika nafasi inayofanana wakati ajali inatokea na ndio maana majeraha yao yanafanana,” amesema dkt Mashala.
Daktari amesema watoto hao walikuwa wanaweza kuzungumza na kujielezea na “hilo lilitupa matumaini makubwa.”
“Kwa hivyo muda wote tukiwa kwenye ndege walikuwa wanatuelezea hali zao basi tunachukua hatua pale wanapokuwa wanahitaji dawa za maumivu,” ameeleza Daktari huyo.
Wakati huohuo wazazi wa watoto hao kwenye mabano Zeituni Abdulkadir (Sadia), Grace Lyimo (Doreen) na Neema Mataba (Wilson) wameeleza shukrani zao kwa watu wa Marekani kwa msaada wao wa hali na mali.
Your browser doesn’t support HTML5
Pia wamesema kuwa wamefarijika sana na maombi ya Watanzania wenzao na watu wote waliokuwa wakiwaliwaza wakati wa tukio la ajali hii.
Wamesema wanamatumaini makubwa kutokana na matibabu watoto hao wanayoyapata kwamba wataweza kurudi Tanzania wakiwa wamepona na wanatembea wenyewe.