Kuachiliwa kwa mateka wa kwanza wanaoshikiliwa na wanamgambo wa Hamas, Gaza kume-ahirishwa hadi Ijumaa, mshauri wa usalama wa taifa la Israeli amesema katika taarifa Jumatano.
Tzachi Hanegbi amesema kwamba kuachiliwa kwa mateka kutaanza kulingana na makubaliano ya awali kati ya wahusika, na sio kabla ya Ijumaa huku mazungumzo juu ya mpango huo yakiendelea.
Hanegbi hakutoa sababu ya kucheleweshwa, na haijafahamika ni lini Israel itaanza mapumziko ya siku nne ya mashambulizi yake Gaza, ambayo yalikuwa sehemu ya makubaliano yaliyotangazwa awali na pande zinazopigana.
Makubaliano hayo yalipangwa kuanza kutekelezwa saa nne asubuhi kwa saa za huko leo hii Alhamisi.
Qatar, ambayo ilisaidia kushughulikia makubaliano hayo pamoja na Marekani na Misri, awali ilisema Hamas, kwa hatua itawaachia wanawake 50 na watoto katika siku zijazo, huku Israel ikiwaachia huru wafungwa 150 wa Kipalestina.