Mataifa manne wanachama wa Afrika Mashariki yametangaza makadirio yao ya bajeti za matumizi ya serikali zao kwa mwaka wa fedha wa 2010-2011.
Mawaziri wa fedha wa nchi za Tanzania,Uganda, Kenya na Rwanda wanawakilisha bajeti katika mabunge ya nchi zao.
Bajeti ya nchi za Afrika mashariki ambayo inasomwa kwa siku moja katika nchi za Kenya Uganda Rwanda na Tanzania imeelezwa kuwa ni njia sahihi ya kuelezea sera za kiuchumi na mipango ya maendeleo ya pamoja ya nchi hizo.
Profesa Samwel Wangwe wa chuo kikuu cha Dar Es Salaam nchini Tanzania amesema itakuwa vigumu kwa nchi ambazo zinaendesha jumuia moja kuwa na tarehe tofauti ya bajeti zao jambo ambalo linaweza kuathiri sera na mipango ya za kiuchumi ya nchi moja na nyingine.
Amesema nchi hizi ambazo zimefikia mkataba wa itifaki wa kuanzishwa kwa soko la pamoja la jumuia hii ni dhahiri kuwa bajeti zao za pamoja ni ishara kuwa zinazingatia maeneo muhimu ya ushirikiano, uondoaji wa Vikwazo vya Kibiashara na uhuru wa kutoa huduma za kibiashara katika Jumuiya na uhuru wa kuhamisha mitaji.
Profesa Wangwe amesema Burundi ambayo imejiunga na jumuia hiyo haina budi kubadili mfumo wake wa bajeti ili iende sambamba na zile za mataifa wanachama wa jumuia hiyo.