Mataifa ya Afrika Magharibi na Kati yatakiwa kuongeza juhudi kupambana na rushwa.

Viongozi wa Jumuiya ya Afrika katika mkutano Addis Ababa.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Amnesty International, limesema Jumanne kwamba mataifa ya Afrika Magharibi na Kati, ni lazima yafanye juhudi za ziada, kupambana na ufisadi na kuacha kuwatesa watetezi wa haki za binadamu, wanaofichua na kushutumu tabia hiyo.

Katika ripoti iliyozinduliwa kwa ajili ya Siku ya Kupambana na Ufisadi barani Afrika, shirika hilo lilishutumu kukamatwa, kunyanyaswa, kuwekwa kizuizini, kutozwa faini kubwa, na hata kuuawa" kwa watetezi wa haki za binadamu wanaopambana na ufisadi katika nchi 19 za Afrika Magharibi na Kati.

Watu hawa wana jukumu muhimu katika kupambana na rushwa na hivyo kutetea haki za binadamu. Katibu mkuu wa Amnesty International Agnes Callamard, amesema mara kwa mara wanakabiliwa na mashambulizi, vitisho, unyanyasaji, na mateso kwa sababu ya kufichua ukweli.

Shirika hilo lilitoa mfano wa mwandishi wa habari wa Cameroon Martinez Zogo, ambaye limesema amekuwa akichunguza madai ya ubadhirifu wa mabilioni ya pesa, unaodaiwa kufanywa na watu walio karibu na serikali.

Zogo alitekwa nyara na watu wasiojulikana Januari 17, na mwili wake baadaye ukapatikana ukiwa umekatwakatwa katika "msitu" nje ya mji mkuu wa nchi hiyo.