Mashambulizi ya Wahodhi yatishia safari za meli bahari ya Sham

Mashambulizi dhidi ya meli za kibiashara katika bahari ya  Sham yanayofanywa na waasi wa Kihouthi, wa Yemen yanasababisha hofu kwa baadhi ya makampuni makubwa ya meli na mafuta.

Hatua hiyo inarudisha nyuma biashara ya kimataifa katika wasaa muhimu wa usambazaji wa bidhaa na nishati ikihatarisha kusababisha ucheleweshaji na kuongeza bei.

Kampuni ya BP, Jumatatu imesema imesitisha kwa muda safari katika bahari ya sham za usafirishaji wa mafuta, gesi asilia na nishati za aina nyingine.

Likielezea kuwa ni hatua ya tahadhari, shirika hilo la mafuta na gesi lenye makao yake London limesema uamuzi huo unafanyiwa uangalizi lakini usalama wa wafanyakazi ni kipaumbele.

Bei za mafuta na gesi asilia za Ulaya zimepanda kutokana na wasiwasi wa mashambulizi ya Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran, ambao walithibitisha mashambulizi mawili mapya Jumatatu.