Maafisa wa Ukraine, Jumatano wamesema shambulizi la anga la Russia, limeuwa takriban watu saba na kuwajeruhi wengine zaidi ya 60 katika mji wa magharibi wa Lviv, ambao Moscow ilikuwa ikiulenga mara chache hapo awali na unapatikana kilomita kadhaa kutoka kwenye uwanja wa mapambano.
Meya wa Lviv, Andriy Sadovyi, amesema katika video iliyowekwa kwenye Telegram kwamba shambulizi hilo limeharibu jengo na mengine zaidi ya 50, ikiwa ni pamoja na shule na nyumba.
Miongoni mwa waliofariki dunia ni watu wanne kutoka familia moja, ambao ni mwanamke mmoja na binti zake watatu, wakimwacha baba yao pekee aliyenusurika.
“Hatutasamehe adui na tutalipiza kisasi,” Sadovyi amesema kwenye Telegram. Russia imeongeza mashambulizi yake ya angani dhidi ya Ukraine, tangu Kyiv ilipoanzisha mashambulizi ya kuvuka mpaka katika eneo la Kursk, Russia, mwezi mmoja uliopita.