Mapigano kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha dharura (RSF) yameingia mwezi wa tatu bila upande wowote kupata ushindi.
Vita hivyo viliwaondoa kwenye makazi yao Wasudani milioni 2.2 na kuua mamia wengine, na kusababisha janga la kibinadamu katika jimbo la Darfur, Umoja wa Mataifa umesema.
Jeshi lina nguvu za anga kwenye ngome zake katika mji wa Khartoum na miji pacha ya Omdurman na Bahri, huku kikosi cha RSF kikijikita katika vitongoji vya makazi ya watu.
Ijumaa na Jumamosi, jeshi lilionekana kuzidisha mashambulizi ya anga, na kushambulia vitongoji kadhaa vya makazi ya watu.
Katika hotuba iliyochapishwa na jeshi siku ya Ijumaa, jenerali wa cheo cha juu Yassir Al-Atta aliwaonya watu kuondoka katika nyumba zinazokaliwa na wapiganaji wa RSF.
“Kwa sababu hivi sasa, tunawashambulia mahali popote walipo,” alisema huku akishangiliwa na watu.
Wizara ya afya ya Khartoum imethibitisha ripoti ya watu wanaojitolea kwamba leo Jumamosi watu 17 wakiwemo watoto watano waliuawa katika eneo la Mayo kusini mwa Khartoum na nyumba 25 ziliharibiwa.