Mashahidi na madaktari wamesema nyumba tatu za huko Rafah zimelengwa na mashambulizi hayo.
Mji wa Rafah uliopo kwenye mpaka kati ya Gaza na Misri kwa sasa unahifadhi zaidi nusu ya wakazi wa Gaza, huku watu wakitafuta makazi wakikimbia operesheni za jeshi la Israel zinazolenga kulitokomeza kundi la wanamgambo wa Hamas.
Jeshi la Israel Jumatatu limesema ndege zake za kivita zilifanya mashambulizi dhidi ya wanamgambo wa Hezbollah kusini mwa Lebanon.
Maafisa wa Hamas walitarajiwa Misri Jumatatu kwa mazungumzo ya karibuni kuhusu pendekezo la sitisho la mapigano la Israel ambalo linajumuisha kusimamisha mapigano kwa kipindi cha wiki kadhaa na kuwaachilia mateka wanaoshikiliwa na Hamas huko Gaza.
Rais wa Marekani Joe Biden na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu walizungumza kwa simu Jumapili kuhusu vita vya karibu miezi saba kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas huko Gaza, lakini White House haikutoa ishara kwamba sitisho la mapigano linakaribia.
Taarifa ya White House imesema viongozi hao wawili “walitathmini mazungumzo yanayoendelea ili kuhakikisha mateka wanaachiliwa pamoja na sitisho la mapigano la mara moja huko Gaza.”