Mashambulizi mapya yametokea Ethiopia, mamia ya watu wameuawa.

Wanajeshi wa Ethiopia wamekabiliana na wapiganaji walioshiriki katika shambulizi baya kabisa magharibi mwa Benishangul – Gumuz, na kuuwa 42 kati yao, kuwapokonya mishale na silaha zingine.

Waziri mkuu Abiy Ahmed amesema kwamba wanajeshi zaidi wametumwa sehemu hiyo inayopakana na Sudan, kuimarisha usalama.

Tukio hilo linajiri siku moja baada ya watu wenye silaha kushambulia Kijiji sehemu hiyo na kuua zaidi ya watu 100.

Ghasia zimekuwa zikitokea Ethiopia tangu Abiy Ahmed alipoteuliwa kuwa waziri mkuu mwaka 2018 na kuanzisha mabadiliko ya kidemokrasia ambayo yalipunguza matumizi ya nguvu dhidi ya wakosoaji wa serikali.

Abiy ameandika ujumbe wa twiter kwamba mauaji hayo ya raia katika Benishangul-Gumuz ni tukio baya sana na kwamba serikali itashughulikia sababu zilizopelekea shambulizi hilo kutokea akiongezea kwamba wanajeshi wametumwa eneo hilo.

Televisheni ya Ethiopia – Fana Tv, imeripoti kwamba wapiganaji 42 wameuawa, bila kutoa maelezo zaidi kuhusu wahusika.

Shirika la kutetea haki za kibinadamu linalosimamiwa na serikali, limesema kwamba zaidi ya watu 100 wameuawa katika shambulizi katika Kijiji cha Bekoji.

Shirika la habari linalomilikiwa na serikali ya Ethiopia limesema kwamba maafisa watano wa ngazi ya juu akiwemo waziri katika jimbo hilo, wamekamatwa kuhusiana na maswala ya usalama wa Benishangul – Gumuz.