Kabla ya mechi kati ya Brazil na Cameroon katika kundi la G kwenye michuano wa Kombe la Dunia huko Qatar, mashabiki walipeperusha bendera kubwa ya Brazil ikiwa na picha ya Pele bingwa wa kandanda wa dunia, wakimtakia afueni ya haraka.
Bingwa huyo wa dunia anapokea hivi sasa matibabu ya kupunguza maumivu baada ya matibabu ya kemotherapi kwa ajili ya saratani ya tumbo kusitishwa.
Pele kupitia ujumbe wa Instagram siku ya Alhamisi aliandika kwamba amelazwa katika hospitali ya Albert Einstien mjini Sao Paulo kwa ajili ya kupimwa na kupatiwa huduma ya kila mwezi, na kuwashukuru mashabiki kwa ujumbe wao kutoka pembe zote za dunia.
Madaktari wanaomtibu Pele wamesema Jumapili kwamba anaendelea vyema kutokana na dawa anazopewa na hali yake haijakuwa mbaya zaidi mnamo saa 24 zilizopita.
Hata hivyo madaktari hao hawakusema kusema chochote kuhusiana na ripoti kwamba bingwa huyo wa kandanda anapewa huduma za “mwisho wa maisha.” Hiyo ni huduma mtu hupewa pale madaktari wanapoamua hakuna tena matumaini ya kuweza kumtibu tena mgonjwa.
Mashabiki wamepeleka ujumbe mbali mbali wakisema “Pele tuko pamoja, tunakutakia kila la kheri, upate afueni ya haraka, daima tuko pamoja.”
“Tumesikitishwa na hali yako hivi sasa, na tuna matumaini utapata afueni ya haraka, lakini hatujui uamuzi wa Mola.”
Pele mwenye umri wa miaka 89, mchezaji pekee wa kandana aliyewahi kushinda mara tatu katika kombe la dunia – 1958, 1962 na 1970 – ni mmoja wa wachezaji kandanda aliyefanikiwa katika mchezo huo na kuwa mashuhuri kote duniani katika karne ya 20.
Akipewa jina la “O Rei” yani Mfalme, alipachika mabao 1 200 katika maisha yake ya kucheza kandanda akiwa mchezaji wa kwanza duniani kufanya hivyo kabla ya kustaafu 1977.