Maseneta saba wa chama cha Democratic wanaiomba kamati ya sheria katika baraza la seneti la Marekani kuwachunguza maseneta wa Republican, Ted Cruz na Josh Hawley kufahamu kikamilifu jukumu lao katika uasi uliofanywa Januari 6 mwaka huu katika jengo la bunge la Marekani na wafuasi wa Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump.
Maelfu ya wafuasi walikusanyika siku hiyo wakati bunge la Marekani lilipokuwa linapiga kura kumuidhinisha rasmi Joe Biden kama mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Novemba 3 mwaka 2020 dhidi ya Trump wakati Hawley na Cruz waliongoza pingamizi katika seneti kutokubali ushindi wa Biden.
Maseneta wa Democratic wanasema Cruz na Hawley walijua madai ya udanganyifu katika upigaji kura hayakuwa na msingi, na yalipelekea vitisho na vurugu. Wa-Democratic wanasema vitendo hivyo vilisababisha waasi kuona wapo sahihi na kupanga vurugu zilizopelekea kuingia ndani ya jengo la bunge. Cruz na Hawley wamelaani vurugu hizo za Januari 6.