Bhavna Patel amekuwa nyanya kwa zaidi ya mwaka mmoja wakati akiishi London, lakini kutokana na kanini zilizowekwa za kutosafiri kwa ajili ya janga, hajaweza kuona mjukuu wake anayeishi New York. Kuanzia Jumatatu, wasafiri kutoka Uingereza pamoja na mataifa mengine wataweza kuingia Marekani, mradi wawe wamepokea chanjo ya covid.
Patel ni mmoja wa mamilioni ya watu ambao hawajaweza kuingia Marekani kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu sasa. Janga la corona limekua na athari kubwa kwa uchumi wa Marekani na sio tu kwenye sekta ya usafiri au utalii.
Todd Knoop ni proesa wa uchumi na biashara kwenye chuo cha Cornell, na anasema kwamba kusafiri au kutosafiri kwa watu huathiri bei za bidhaa kwa namna moja ama nyingine,hali ambayo hushuhudiwa karibu kwenye kila sekta ya kiuchumi.
Profesa Todd anasema kwamba sekta ya utalii wa ndani wa Marekani imesaidia uchumi kinyume na baadhi ya mataifa mengine ambayo hutegemea watalii kutoka nje.
Kuna matatizo ya misongamano kama ile ya meli inayoshuhudiwa kwenye bandari za Long Beach na Los Angeles. Meli kwenye ufukwe wa magharibi mwa Marekani zinalazimika kusubiri kwa siku nyingi kabla ya kushusha mizigo, nyingi zikitokea China na Uingereza.
Kwa wasafiri kama Bhavna Patel, habari njema kwake sasa ni safari anayosubiri kuelekea New York ili kumuona binti yake. Anasema kwamba amejawa na furaha tele. Kando na safari za ndege, Marekani leo Jumatatu imefungua safari za barabara kwenye mipaka ya Mexico na Canada, kwa watu waliopokewa chanjo za Covid.