Maria Sarungi azungumzia jaribio la kutekwa nyara Kenya

Mwanahabari na mwanaharakati Maria Sarungi. Picha na Zainab Said

Mwanahabari na mwanaharakati Maria Sarungi hatimaye amevunja ukimya kufuatia jaribio la kumteka nyara siku ya jumapili Nairobi, Kenya

Mwanahabari na mwanaharakati Maria Sarungi hatimaye amevunja ukimya kufuatia jaribio la kutekwa nyara siku ya Jumapili Nairobi, Kenya

Akizungumza na wanahabari Maria amehushisha kitendo hicho na semi za kuikashifu serikali ya Tanzania ya Rais Samia Suluhu Hassan hasa wakati huu ambao taifa hilo linajiandaa kwa uchaguzi mkuu.

Maria ameapa kutositisha mwenendo wake wa kuikashifu serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi mbaya, amesimulia matukio aliyopitia mikononi mwa wanaume watatu waliomteka nyara majira ya saa tisa mchana saa za Afrika Mashariki alipokuwa akitoka saluni.

Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii amekuwa akiikashifu serikali ya rais Samia Suluhu akisema iwapo nia ya kisa hicho ni kumtia uoga basi halijafaulu na kuwa ataendelea kuyataja maovu ya serikali.

Mkosoaji huyo mkubwa wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, anasema kumbukizi za matukio aliyopitia mikononi mwa wanaume watatu waliokuwa wamemteka nyara na mazungumzo kati yao ni udhihirisho lengo lilikuwa kumvusha kutoka Kenya hadi Tanzania ila jaribio hilo halikufanikiwa baada ya taarifa za kutojulikana aliko kusambaa mitandaoni na sasa anatoa wito kwa jamii ya kimataifa kufuatilia kwa ukaribu kile anachokitaja ni ukiukaji wa haki za binadamu nchini humo.

Si mara ya kwanza kwa tukio kama hili kutokea nchini kumekuwa na matukio kadhaa ya raia wa kigeni wanaotafuta hifadhi nchini Kenya kutekwa nyara na kulazimishwa kurudi katika mataifa yao bila hiari yao.

Tukio la hivi majuzi ni kuhusiana na kiongozi wa upinzani Uganda Kiza Besigye alitekwa nyara akiwa katika shughuli binafsi nchini Kenya na kisha baadae kupatikana nchini Uganda alipofikishwa katika mahakama ya jeshi nchini humo.

Sasa shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International linaonya mwenendo huu hauchafui tu sura ya Kenya kimataifa bali pia inahatarisha demokrasia katika mataifa ya ukanda wa Afrika Mashariki.

Hakuna taarifa iliyotolewa na serikali ya Kenya au Tanzania wakati tukienda hewani kuhusiana na tukio hilo.

Tukio hili linajiri huku vumbi la utekaji nyara nchini Kenya llikiendelea kutifuka.

Serikali ya Rais William Ruto imekuwa ikikashifiwa kwa kuendeleza visa vya utekaji nyara na hata kupotea kwa wanaokashifu uongozi wake tangu kufanyika maadamano ya vijana mwezi Juni mwaka jana.

Semi za hivi majuzi za kuilaani serikali ya rais Ruto zimetolewa na mmoja wa waziri katika baraza lake.

Imetayarishwa na Zainab Said,Sauti ya Amerika Nairobi