Marekani yawawekea vikwazo maafisa 16 wa serikali ya Venezuela

  • VOA News

Rais wa Venezuela Nicholas Maduro

Marekani Alhamisi ilitangaza msururu wa vikwazo dhidi ya serikali ya Rais wa Venezuela Nicolas Maduro.

Hatua hiyo inajiri zaidi ya mwezi mmoja baada ya uchaguzi wa rais wenye utata wa Julai 28 nchini Venezuela na siku kadhaa baada ya mgombea wa upinzani, Edmundo Gonzalez kuondoka nchini na kuomba hifadhi nchini Uhispania.

Kulingana na afisa mkuu wa utawala wa Biden ambaye aliwapa taarifa hiyo waandishi wa habari, wizara ya fedha iliwawekea vikwazo maafisa 16 washirika wa Maduro, wakiwemo viongozi wa Baraza la kitaifa la uchaguzi, mkurugenzi wa Baraza hilo Rosalba Gil, na mkuu wa Mahakama ya Juu Caryslia Rodriguez.

Afisa huyo mkuu alisema maafisa hao wanashtumiwa kufanya unyanyasaji wa haki za binadamu na maafisa wa jeshi na idara ya ujasusi walichukuliwa pia vikwazo kwa kuhusika kwao katika ukandamizaji wa baada ya uchaguzi.

Serikali ya Maduro ilijibu katika taarifa ikisema “ Venezuela inapinga vikali uhalifu mpya wa uchokozi unaofanywa na serikali ya Marekani dhidi ya Venezuela kwa kuchukua hatua za kulazimisha za upande mmoja.”