“Watu wanaweza kuwa na imani kubwa kwamba chanjo hii inakidhi viwango vya juu vya usalama, ufanisi na ubora wa utengenezaji ambao FDA inahitaji kwa bidhaa iliyoidhinishwa,” kaimu kiongozi wa FDA Janet Woodcock amesema Jumatatu katika taarifa.
Saa chache baada ya idhini hiyo, Rais wa Marekani Joe Biden amewahimiza Wamarekani kuchanjwa, akisisitiza kuhusu usalama na ufanisi wa chanjo.
“Naomba niseme wazi na kwa sauti kubwa, ikiwa wewe ni miongoni mwa mamillioni ya Wamarekani waliosema kwamba hawatachanjwa hadi pale FDA itakapotoa idhini kamili, hili sasa limefanyika,” Biden amesema.
“Wakati uliokuwa unasubiri nii huu. Ni wakati wa kupokea chanjo yako,” Biden ameongeza.
Chanjo inayotengenezwa na kampuni ya Pfizer-BioNTECH iliidhinishwa kwa matumizi ya dharura mwezi Disemba mwaka jana.
Baadhi ya wataalamu wanatumai kwamba idhini kamili itawahamasisha watu wengi wanaosita kupewa chanjo kuchanjwa, hasa wakati huu, ambapo Marekani inapambana na ongezeko kubwa la maambukizi linalochochewa na aina ya virusi vya Detla vinavyoambukiza kwa kasi.