Marekani yatangaza vikwazo dhidi ya kundi la mamluki wa Russia, Wagner na washirika wa kundi hilo

Kituo cha kundi la Wagner, mjini Saint Petersburg, Russia

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken Alhamisi alitangaza msururu wa vikwazo vinavyowalenga watu wanaohusishwa na kundi la kijeshi la Russia, Wagner, akiwemo kiongozi wa kundi hilo na makampuni washirika wa Wagner, kwa kuhusika katika vita dhidi ya Ukraine.

Katika taarifa, Blinken alisema vikwazo hivyo vitalenga kampuni tano na mtu mmoja mwenye uhusiano na Wagner na kiongozi wa kundi hilo, Yevgeniy Prigozhin, vile vile watu wengine kadhaa na mashirika, kwa hadhi yao kama maafisa wa serikali na kuwa sehemu ya sekta ya viwanda vya zana za kijeshi za Russia.

Taarifa ya Blinken imesema wizara ya mambo ya nje imewataja pia watu watatu kwa majukumu yao kama wakuu wa idara ya magereza ya Russia, ambayo imekuwa ikiripotiwa kurahisisha kuajiri wafungwa wa Russia kujiunga na kundi la Wagner, na baadaye kupelekwa kwenye uwanja wa mapambano kupigana katika mzozo wa Ukraine.