Marekani yapongeza kuachiwa raia wake kutoka Iran

Mabaharia wa Marekani walioachiwa na Iran, Januari 13, 2016

Marekani imepongeza kuachiliwa kwa mabaharia 10 wa jeshi la majini la Marekani siku ya Jumatano siku moja baada ya kuingia kwenye mipaka ya majini ya Iran na kukamatwa.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry, alisema suluhisho la tukio hilo ni mafanikio ya kidiplomasia na Waziri wa Ulinzi wa Marekani,Ash Carter alisema alifurahi kuona wanajeshi hao “wanarudi mikononi mwetu”. Maafisa wa marekani bado hawana uhakika na kilichosababisha kwa mabaharia hao kukamatwa, alisema bwana Carter kwa sababu bado hawajaweza kuwasiliana kikamilifu na mabaharia hao.

Mabaharia hao walioachiwa huru, tisa ni wanaume na mmoja mwanamke ambapo hivi sasa wapo kwenye kituo cha Marekani huko Qatar. Iran pia iliachia boti mbili ndogo za doria za Marekani walizotumia wakati walipokamatwa.

Waziri wa ulinzi wa Marekani, Ash Carter.

Wafanyakazi hao walikuwa wakisafiri kupitia ghuba ya Uajemi kutoka Kuwait kuelekea Bahrain wakati wafuatiliaji misafara wa Marekani walipopoteza mawasiliano nao siku ya Jumanne. Kikosi cha Ulinzi wa Mapinduzi ya Iran ambacho kinafanya doria kwenye ghuba kilikamata boti hizo na wafanyakazi wake karibu na kisiwa cha Farsi, ardhi ya Iran iliyopo kati kati ya Kuwait na Bahrain.

Wakati huo huo ofisa mmoja wa ulinzi wa Marekani aliiambia Sauti ya Amerika-VOA kwamba wafuatiliaji safari za majini walipoteza mawasiliano na wafanyakazi hao kwenye boti zote mbili za doria.