Marekani yaombwa kuondolea Zimbabwe vikwazo

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Alhamisi ameiomba Marekani kuondoa vikwazo dhidi ya Zimbabwe akisema kwamba vimeongeza janga la kibinadamu pamoja na kudorora kwa uchumi, wakati akipendekeza kuwepo kwa mashauriano ili kumaliza uhasama uliopo. 

Alena Douhan ambaye ni mjumbe maalum wa UN wa masuala yanayohusiana na vikwazo na amekuwepo nchini Zimbabwe kwa karibu wiki mbili sasa wakati akitathmini athari zitokanazo na vikwazo vya Marekani kwenye taifa hilo la kusini mwa Afrika.

Marekani iliweka vikwazo vya kifedha na vya kusafiri kwa baadhi ya viongozi wa kisiasa na kijeshi pamoja na wafanyabiashara yakiwemo makampuni yanayohusishwa na serikali, takriban miongo miwili iliyopita.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AP hatua hiyo ilichukuliwa baada ya wakulima wa kizungu kupokonywa mashamba yao pamoja na wizi wa kura na ukiukaji wa haki za binadamu kutoka kwa kiongozi wa muda mrefu marehemu Robert Mugabe.

Ubalozi wa Marekani mapema wiki hii umesema kwamba unaweza kuondoa vikwazo hivyo baada ya kuthibitisha kwamba watu waliowekewa wameacha kuhujumu demokrasia, kushiriki ufisadi pamoja kukiuka haki za kibinadamu.