Marekani yakiri kuua raia katika shambulizi la Somalia

Raia wa Somalia katika eneo la shambulizi.

Marekani imesema kwamba raia mmoja aliuawa na wengine watatu kujeruhiwa katika shambulizi la angani lililotekelezwa na jeshi lake mwezi Februari mwaka huu.

Hii ni mara ya pili jeshi la Marekani kukiri kuua na kujeruhi raia tangu lilipoanza kutoa ripoti zake kuhusu mauaji ya raia katika shughuli zake za kijeshi barani Afrika.

Katika ripoti ya hivi punde, kituo cha jeshi la Marekani lenye barani humo –AFRICOM, kimesema kwamba ukweli kuhusu shambulizi lililotekelezwa Februari tarehe 2, unaonyesha kwamba raia mmoja aliuawa na wengine watatu kujeruhiwa.

Kikosi cha Africom hata hivyo kimesema kwamba mauaji hayo hayakutokea maksudi na kwamba kinafanya kazi kwa uangalifu mkubwa kuzuia vifo au majeruhi kwa raia.

Shambulizi hilo lilitokea katika sehemu ya Jilib, karibu kilomita 380 kusini mwa mji mkuu wa Somalia – Mogadishu.

Ripoti ya AFRICOM kuhusu mauaji na majeruhi ya raia inaangazia operesheni zake katika nchi za Somalia, Libya na nchi zingine za Afrika.

Ripoti ya kwanza iliyochapishwa mwezi April, ilieleza kwamba raia wawili waliuawa katika shambulizi la angani la mapema mwaka 2019.

Jeshi la Marekani limekuwa likitekeleza mashambulizi nchini Somalia kwa kipindi cha miaka mingi katika juhudi za kulishinda nguvu kundi la wapiganaji la Al-shabaab.

Makundi ya kutetea haki za kibinadamu yamekuwa yakishutumu Marekani kwa kutekeleza operesheni zake nchini Somalia kwa usiri mkubwa na kufanya vigumu kupata ripoti za uajibikaji iwapo kuna ajali zinatokea, na hasa kuhusu vifo vya raia.

-Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC