Marekani yakanusha madai ya Sudan Kusini

Rais wa Sudan Salva Kiir

Balozi mpya wa Marekani kwa Sudan Kusini amekanusha shutuma ambazo zimetolewa na utawala wa Kiir kwamba Marekani inataka mabadiliko ya uongozi nchini Sudan Kusini.

Balozi Thomas Hushek anasema Marekani inataka kuona amani inarejea baada ya takriban miaka minne na nusu ya mapigano.

Katika mahojiano maalum Jumatano na Sauti ya Amerika, balozi Hushek amesema Marekani inataka kuona kuwa ghasia zinamalizwa na itaendelea kuwa nyuma ya watu wa Sudan Kusini.

“Tungependa kuona mabadiliko katika tabia ya viongozi wote katika serikali na nje ya serikali ili kulenga na kufanikisha amani,” amesema.

Kufanikisha lengo hilo, Hushek amesema, Marekani itatumia mbinu ambazo zinajumuisha vikwazo maalum pamoja na mbinu kama vile kuwahusisha watu wa Sudan Kusini na viongozi.

Waziri wa habari wa Sudan Kusini, Michael Makuei, mara kwa mara ameishutumu Marekani kuwa inataka kuona serikali ya Juba inabadilishwa.

“kwetu sisi kama serikali, hili si jambo jipya. Huu ni muendelezo wa sera ya mabadiliko ya utawala. Kwetu sisi hili si suala,” amewaambia wana habari mwishoni mwa mwezi Mei mjini Juba.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hivi karibuni liliendeleza vikwazo kwa siku 45 za ziada kwa ajli ya Sudan Kusini kutokana na juhudi ambazo zimeongozwa na Marekani. Baraza, hata hivyo, limechelewesha uamuzi kwa siku 30 kuweka marufuku ya kusafiri na kuzuia mali kwa viongozi sita wa Sudan Kusini wanaoshutumiwa kuzuia juhudi za amani. Baraza limesema hatua hiyo bado iko mezani ikisubiriwa tathmini ya nia ya dhati kwa pande zote kutekeleza mkataba wa sitisho la mapigano ambao walitia saini mwezi Desemba mwaka 2017.

Kama Washington haitapata uungaji mkono wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, au taasisi ya kieneo IGAD, Marekani huenda ikaweka vikwazo hivyo peke yake, Hushek ameonya.

Mzozo wa Sudan Kusini ulianza mwaka 2013 ikiwa ni mapambano ya madaraka kati ya Rais Salva Kiir na naibu wake wa zamani, Riek Machar. Mzozo umesababisha zaidi ya raia milioni 4 wa Sudan Kusini kukimbia makazi yao na kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya nusu ya idadi ya watu, au watu milioni saba, wanahitaji msaada wa kibinadamu. Sudan Kusini ni nchi changa sana duniani.